Aliyewahi kuwa kocha wa Simba James Aggrey Siang’a amefariki leo alfajiri nchini kwake Bungoma nchini Kenya baada ya kuugua kwa muda mrefu. Siang’a alikuwa ni miongoni mwa makocha walioheshimika sana Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa afisa wa Chama cha Kefoca, Bob Oyugi, Siang’a ambaye aliwahi kuchezea Gor Mahia, Luo Union na timu ya taifa Kenya Harambee Stars kama kipa, pia aliwahi kuwa kocha wa klabu za Simba, Moro United na Express ya Uganda.
Siang’a aliidakia Kenya katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1972 na pia alikuwa kocha wa Harambee Stars mwaka 1999 na 2000, kabla ya kuhamia Tanzania kufundisha Simba, Mtibwa Sugar, Moro United na timu ya taifa ya Bara kwa muda mfupi mwaka 2002.
Mashabiki wa Simba SC watamkumbuka zaidi Sianga baada ya kuipa timu taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati visiwani Zanzibar mwaka 2002, kabla ya kuunda kikosi imara cha vijana wadogo kilichokuwa tishio katika soka ya Tanzania muongo wote huo.
Akiwa na Moro United Oktoba 2004 Siang’a aliombwa kuinoa Taifa Stars lakini alikataa. Siang’a pia aliinoa Mtibwa Sugar kabla ya kurejea Kenya kuifundisha timu ya Gor Mahia.
Siang’a ndiye aliyeiwezeha Simba SC kuitoa Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa wa Afrika katika hatua ya 16 Bora na kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tumempoteza mtu wetu sana, Siang’a. Mchezaji wa zamani wa kimataifa amefariki ijumaa usiku kwa mujibu wa familia yake. Tunasubiri taarifa zaidi kutoka kwao ili kuendelea na hatua nyingine. Mwili wake upumzishwe kwa amani,” alisema Oyugi.
Kikosi hicho kilikuwa kikiundwa na vijana kama Said Swedi, Ramazani Wasso, Boniface Pawasa, Victor Costa, Lubigisa Madata, Suleiman Matola, Primus Kasonzo, Christopher Alex, Shekhan Rashid, Ulimboka Mwakingwe, Emmanuel Gabriel na Athumani Machuppa.
Sianga alizitoa BDF XI ya Botswana, Santos ya Afrika Kusini kabla ya Zamalek. Santos aliitoa kwa penalti 9-8 baada ya sare ya jumla 0-0 na Zamalek pia aliitoa kwa penaliti 3-2, baada ya sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
Simba ikapangwa Kundi A pamoja na Ismailia ya Misri, Enyimba ya Nigeria na ASEC ya Ivory Coast na ikafanikiwa kushinda mchi mbili na kutoa sare moja.
Ilishinda 1-0 dhidi ya ASEC, 2-1 dhidi ya Enyimba na sare ya 0-0 na Ismailia katika mechi za nyumbani Uwanja wa Taifa, (sasa Uhuru), Dar es Salaam.
Katika mechi za ugenini, Simba SC ilifungwa 3-0 na Enyimba, 2-1 na Ismaili na 4-3 na ASEC. Kituko kikubwa cha kukumbukwa cha Siang’a ni pale alipompiga kichwa aliyekuwa kocha wa SC Villa, Mserbia Milutin Sredejevic ‘Micho’ kwenye fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Simba SC ikilala 1-0 Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, Uganda.
Micho alikwenda kwenye benchi la Simba kumsalimia Siang’a aliyekuwa ana hasira za kipigo na kukosa Kombe na pia akilalamikia bao la Mkenya mwenzake, Vincent Tendwa aliyemalizia krosi ya kiungo Mtanzania, Shaaban Kisiga ‘Malone’ lilikuwa la kuotea – lakini akaambulia ‘ndoo’.
Kabla ya Micho kujibu, wawili hao wakatenganishwa na sherehe za ubingwa zikachukua nafasi yake Namboole.
Baada ya kuondoka Simba alifichua mpango wa kufuatwa na kiongozi mmoja wa klabu wakati huo kumshawishi wapokee hongo ya Zamalek timu ifungwe mwaka 2003.
Siang’a alidai alikataa na akaiongoza Simba kuitoa Zamalek, lakini kilichofuatwa ni kufukuzwa kwenye timu kwa chuki za kiongozi huyo mwenye asili ya Kiasia. Mungu ampumzishe kwa amani gwiji huyo wa soka Kenya.
GPL
No comments:
Post a Comment